Tuesday, October 23, 2012

WAKRISTO GEITA WACHARUKA WADAI HAWAKO TAYARI KUCHOMEWA MAKANISA
Na
MAGRETH CHABA
UMOJA wa makanisa ya kikristo ya Katoro wilayani Geita na Buseresere wilayani Chato,mkoani Geita umecharuka na kulaani kitendo cha hivi karibuni kilichofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu cha kuchoma moto makanisa na kuharibu mali za wakiristo.

Kitendo hicho kilisababisha vurugu kubwa zilizotokea  oktoba 12 mwaka huu Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam ambapo makanisa saba yalichomwa moto kutokana na kitendo kinachodaiwa na mtoto mwenye umri wa miaka 14 kukojolea Quran.

Umoja huo umetoa tamko kuhusiana na kitendo hicho katika mkutano wa uliofanyika juzi mjini Katoro na kuwakutanisha waumini wa madhehebu mbalimbali ya kikristo pamoja na viongozi wao.

Akitoa tamko hilo mwenyekiti wa umoja huo,Mchungaji Joseph Mwanzalima Hewa,alisema serikali ikishindwa kudhibiti matukio ya vurugu za waislamu kujichukulia sheria mkononi kutokana na udini taifa halitakuwa na amani.

Alisema kuna hatari ya taifa,linaweza kuingia katika umwagaji wa damu kwani kitendo hicho hakivumiliki kwa wakristo kuzidi kupumbazika kwa kuharibiwa mali zao.

Hewa alisema zaidi ya biblia 50 ziliwahi kuchomwa moto lakini wakristo hawakuchukua hatua zozote dhidi ya wahusika wala hakuna msikiti uliochomwa moto na kwamba hakuna vurugu zilizotokea na hivyo kuhoji uhalali wa waislamu kuiweka nchi kwenye rehani ya vita ya kidini.

Alisema serikali inapaswa kuingilia kati kukomesha matukio hayo yanayofanywa na baadhi ya makundi ya waumini wa dini ya kiislamu ili nchi iendelee kuwa kisiwa cha amani.

Aidha alisema kama serikali itashindwa kudhibiti matukio hayo,hawatavumilia kuendelea kuharibiwa makanisa yao na kudai kuwa wako tayari kufa wakitetea haki zao.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa waliohusika katika matukio hayo wanapaswa kuchukulia hatua kali za kisheria akiwemo kinara wa kikundi cha Uamsho kisiwani Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed.

''Serikali imekuwa ikiwakumbatia waislamu sasa tunasema yatosha,hatuwezi kuona mali zetu zinaharibiwa,kama itakuwa kimiya katika hili nchi itaingia katika vurugu kubwa na vita kutokana na udini ulioanza kujipenyeza''alisema Hewa.

Naye aliyewahi kuwa mwenyekiti wa umoja huo Isaya Ikili alisema anasikitishwa na watendaji wa kata pamoja na viongozi wa serikali kushindwa kuhudhuria katika mkutano huo licha kupewa mwaliko ili kujua matamko yao.

Alisema wako tayari kupambana na maadui wao wanaoharibu makanisa yao na kwamba polisi wasiingilie vurugu hizo kama serikali itashindwa kuyadhibiti.
                                                                            MWISHO.

MW/KITI CCM GEITA APIGWA STOP MGODINI AKIENDA KUZINDUA KAMPENI
Na                           
Magreth chaba

VIGOGO wa chama cha mapinduzi(ccm)mkoani Geita waliochaguliwa hivi karibuni ,akiwemo mwenyekiti wa mkoani ,Joseph Msukuma wameonja machungu ya mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM)baada ya msafara wao kuzuiliwa kwa muda wakati wakielekea kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo.

Tukio la kuzuiliwa kwa viongozi hao lilitokea jana mchana saa 7:03 kutokana na kile kilichodaiwa na walinzi wa mgodi huo kampuni ya G4S waliokuwa wamefura hawakuwa na taarifa za viongozi hao kupita mgodini hapo kitendo kilichosababisha majibizano makali ya maneno kati ya walinzi hao na vigogo hao.

Mwenyekiti huyo alikumbwa na kizazaa hicho akiwa na katibu wa itikadi na uenezi mkoa Said Kalidushi na katibu wa uchumi na fedha mkoa Malugu Mwendesha walipokuwa wakielekea katika kuzindua  kampeni za uchaguzi mdogo wa kata ya Lwezera tarafa ya Bugando.

Baada ya kuzuiliwa Msukuma alijitambulisha kwa walinzi kuwa ni mwenyekiti wa ccm mkoa huku akiwaonyesha bendera ya chama iliyokuwa ikipepea kwenye gari lake lenye namba za usajili T 164 AFQ aina ya Toyota V-8 lakini walinzi walisema wao wanafuata sheria za uongozi wa mgodi huo na kwamba hawakuwa tayari kuruhu kupita kwa kuwa hawakupewa na taarifa.

Msukuma alisikika akiwakaripia maneno walinzi hao’’serikali Unayoitaka wewe ni ipi,tueleweshe ama unataka ya chama gani huoni hata bendera,kila siku napita hapa huwa hamnioni na hili gari ’’

Naye mlinzi mmoja alisikika akisema’’sisi tunafuata taratibu zilizopo,kwani mnaelekea wapi?,sisi hata kama ni kiongozi wa serikali anapofika hapa huwa tunataarifiwa lakini sasa hatuJajulishwa’’

Kufuatia maneno hayo ya mwenyekiti,mlinzi mmoja alijitokeza na kulazimika kupiga simu mgodini kuuliza kuhusu kumruhusu kupita ambapo wakati akifanya mawasiliano hayo mlinzi huyo alisikika akizitaya namba za gari hilo.

Mlinzi huyo baada ya kuwasiliana na uongozi wa mgodi huo na kuruhusiwa viongozi hao kupita saa 7:25,mmoja wao alisema’’tunaomba samahani kama tumewachelewesha sisi tunafuata taratibu za uongozi wa mgodi’’.

Aidha akiwa katika uzinduzi wa kampeni hizo mwenyekiti wa aliwataka wananchi wa kata hiyo kumchagua mgombea wa ccm Misango Jeremiah ili kuwaletea maendeleo katika kata hiyo ikiwemo huduma ya afya barabara na ofisi ya kata hiyo.

Kampeni za uchaguzi huo unaotarajia kufanyika oktoba 28 mwaka huu unakuja kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo Anatori Mkufu aliyefariki februari 23,mwaka huu kwa ajali ya gari akiwa jijini Mwanza.
                                                                    MWISHO.

Wednesday, October 3, 2012

ASKARI WAPATA KASHFA NZITO

Na Magreth Chaba,Chato.
ASKARI wa kituo kidogo cha Polisi cha Buziku wilayani Chato mkoani Geita wamekumbwa na kashfa kubwa baada ya kutuhumiwa kuwakamata na kuwatesa wananchi wawili waliokuwa wamelala kwenye nyumba ya wageni ya Buziku Hill Guest House hali iliyosababisha mmoja wao kupoteza maisha.
Tukio hilo limetokea Oktoba 30 mwaka huu majira ya saa 5;30 usiku wakati wananchi hao wakiwa wamejifungia ndani ya vyumba vyao wakiendelea kunywa pombe(Bia) ambapo askari polisi walifika eneo hilo na kuwaamuru kufungua milango yao kwa lengo la kuwafanyia upekuzi.
Baada ya wananchi hao kukaidi amri ya polisi,askari hao walilazimika kutumia nguvu na kufanikiwa kuvunja milango ya vyumba hivyo kisha kuanza kuwaadhibu watu hao kabla ya kuwapeleka kwenye kituo kidogo cha polisi kilichopo kwenye kata hiyo.
Aidha ameelezwa kuwa baada ya kipigo kikali vijana hao walipelekwa kwenye kituo hicho cha polisi na kabla ya kuhojiwa hali zao kiafya zilibadilika ghafra na kulazimika kuwakimbiza kwenye Kituo cha afya cha Bwanga kwaajili ya matibabu lakini kutokana na kuonekana mahututi zaidi walikimbizwa hospitali ya wilaya ya chato.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Paulo Kasabago amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa askari wake walifika eneo la tukio baada ya kuelezwa na raia mwema kuwa kuna watu wanaosadikiwa ni majambazi kutokana na mazungumzo waliyokuwa nayo wakati wakinywa pombe nje ya guest hiyo kabla ya kuingia ndan ya vyumba vyao kulala.
Ameeleza kuwa baada ya askari wake kuingia ndani kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa na kuwafanyia upekuzi,mmoja wa watuhumiwa hao alimkwida koo askari PC Mwidin hali iliyosababisha askari wenzake kutumia nguvu kubwa ili kumsuru mwenzao kujeruhiwa.
Amesema baada ya kufanikiwa kuwatoa ndani ya vyumba vyao na kabla ya kuwafikisha kituoni,kundi kubwa la wananchi waliokuwa wanatoka kutazama soka la ulaya kwenye moja ya ukumbi uliopo kijijini hapo walifika kwenye tukio na kuanza kuwasaidia polisi kuwapeleka watuhumiwa hao lakini kutokana na kukataa kata kata wananchi walianza kuwaadhibu huku mkuu wa kituo hicho cha polisi akilazimika kuwazuia.
Baada ya kumalizika upekuzi wa askari walifanikiwa kukuta kiasi cha shilingi laki 5 ndani ya chumba kimoja na kingine walikuta kiroba cha mfuko uliokuwa na mawe yanayosadikiwa kuwa ni ya dhahabu pamoja na chupa moja ya pombe aina ya Bia.
Kadhalika wakati watuhumiwa hao wakiendela kupata matibabu kwenye hospitali ya wilaya ya chato,mmoja wao alifariki dunia wakati akiendelea kutibiwa.
Kasabago amemtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Gilbert Ntabonwa mkazi wa kijiji cha Kakeneno na mzaliwa wa Kibondo mkoani Kigoma huku majeruhi mwingine David Vyamana hali yake ikiendelea vizuri.
Kufuatia hali hiyo jeshi hilo linawashikilia askari wake wanne kwaajili ya uchunguzi kutokana na kutuhumiwa na kuhusika na tukio la kujeruhi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kwamba uchunguzi utakapo kamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.
Amewataja askari wanaoshikiliwa kuwa ni OCS wa kituo hicho Sajent Raulens Bendera,PC Mwidin,PC abdalah na PC Yusuph wote wakiwa ni askari wa kituo kidogo cha Buziku.
Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Chato Dk Pius Buchukundi amekiri mmoja wa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kufariki dunia wakati akiendelea na matibabu.
Amesema uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa marehemu alikuwa amejeruhiwa vibaya kutokana na kipigo hali iliyosababisha damu kuvujia ndani ya mwili na hivyo kupelekea mauti hayo.
Mwisho.